Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, katika kikao chake na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Taeb, Mkuu wa Shirika la Basij la Wanyonge, kilichofanyika jana mjini Qum, alizungumzia uwezo mkubwa wa Basij katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kisayansi na kiuchumi, na kusisitiza mambo sita ya kimkakati kwa ajili ya kuimarisha shughuli za taasisi hii.
Mkurugenzi wa Hawza za kielimu, akieleza kuwa Basij ina uwezo wa kipekee wa kuleta mabadiliko katika jamii, alisema: “Uzoefu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kipindi cha Ulinzi Mtakatifu na mabadiliko pamoja na matukio ya hivi karibuni, umeonesha kuwa kila mara hisia za ushiriki na uwajibikaji zinapoimarishwa miongoni mwa wananchi, hususan kizazi cha vijana balehe na vijana, uwezo mkubwa uliopo ndani ya jamii huanza kufanya kazi.”
Mihimili sita ya msingi ya kuhuisha uwezo wa Basij
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za kielimu nchini Iran, akisisitiza kuwa Basij inapaswa kuhuisha na kuimarisha uwezo wake kulingana na mazingira mapya ya jamii, alifafanua mihimili sita ya msingi katika suala hili.
1. Mhimili wa kwanza: Kuimarisha hisia za ushiriki na kuwafanya vijana wajione kuwa wanashiriki katika hatima ya nchi
Ayatullah Arafi alilitaja jambo la kwanza kuwa ni ulazima wa kuchochea hisia za ushiriki miongoni mwa vijana balehe na vijana wa makamo, akisema: “Ushiriki pekee hautoshi; jambo muhimu zaidi ni kujenga hisia za ushiriki na kujiona kuwa sehemu ya jambo husika miongoni mwa watu. Kizazi cha vijana balehe na vijana wa makamo kinapaswa kuhisi kuwa kina nafasi katika ujenzi wa nchi, maendeleo ya jamii na mabadiliko ya Mapinduzi ya Kiislamu, na kwamba si watazamaji tu wa matukio.”
2. Mhimili wa pili: Kuzalisha mfumo wa fikra na lugha yenye mvuto kwa ajili ya kuongoza na kuchochea harakati za kijamii
Mkurugenzi wa Hawza za kielimu, katika kufafanua jambo la pili, alisisitiza ulazima wa shughuli za kijamii kuwa na mfumo wa fikra, nadharia na lugha inayolingana nazo, akisema: “Moja ya sababu za mafanikio ya kila harakati ya kijamii ni kuwa na mfumo wa fikra na lugha inayoweza kuwasiliana na nafsi na hisia za walengwa, kuwachochea na kuwaweka wazi kuhusu njia ya harakati.”
3. Mhimili wa tatu: Kujiandaa kukabiliana na mabadiliko ya Akili Unde na Sayansi za Utambuzi
Ayatullah Arafi, katika kueleza mhimili wa tatu, akizungumzia mabadiliko makubwa ya anga za mtandao, Akili Unde na Sayansi za Utambuzi, alionya kuhusu misukosuko ya kisayansi na kiutamaduni inayokuja, akisema: “Mabadiliko yaliyotokea katika anga za mtandao yameambatana na athari nyingi chanya na hasi; tumefaidika na baadhi ya fursa zake na wakati huohuo tumepata madhara pia, lakini kile kinachotukabili sasa ni mabadiliko ya kina zaidi katika nyanja za Akili Unde na Sayansi za Utambuzi.”
4. Mhimili wa nne: Kulinda hazina ya wasomi nchini na kubuni mfumo wa kuwaongoza wenye vipaji vya hali ya juu
Mkurugenzi wa Hawza za kielimu, katika kueleza mhimili wa nne, alisisitiza ulazima wa kuwajali kwa dhati wasomi na wenye vipaji vya hali ya juu nchini, akisema: “Suala la wasomi na wenye vipaji vya hali ya juu ni miongoni mwa masuala ambayo yanapaswa kuendelea kuzingatiwa na viongozi. Msomi mmoja anaweza, peke yake, kuwa na ushawishi katika hatima na mabadiliko ya nchi, na tofauti ya kuwepo au kutokuwepo watu wa aina hii katika nafasi za kisayansi na kiutawala ni yenye umuhimu mkubwa sana.”
5. Mhimili wa tano: Kuamsha uwezo wa wananchi na kuwepo fikra za Basij katika nyanja ya uchumi
Ayatullah Arafi, katika kufafanua mhimili wa tano, huku akisisitiza ulazima wa kukabidhi shughuli za kiuchumi na sekta mbalimbali za jamii kwa wananchi na sekta binafsi, alisema: “Moja ya misingi muhimu katika kuendesha nchi ni wananchi kuwepo katika uwanja wa shughuli na kwamba shughuli za kiuchumi na kijamii ziendelee, kadiri inavyowezekana, kwa ushiriki na ubunifu wao.”
6. Mhimili wa sita: Kuimarisha mwelekeo wa kimataifa na kutumia fursa ya kipekee ya kimataifa kwa ajili ya kufafanua Mapinduzi ya Kiislamu
Mkurugenzi wa Hawza za kielimu, katika kueleza mhimili wa sita, huku akizungumzia mazingira mapya ya kimataifa na kuongezeka kwa umakini wa maoni ya umma duniani kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: “Katika uwanja wa kimataifa, mabadiliko mapya yanaendelea kujitokeza, na mazingira ya sasa ya nchi na Mapinduzi ya Kiislamu, licha ya uadui mkubwa wa Marekani na baadhi ya serikali zinazoshirikiana nayo, yameandaa fursa muhimu kwa ajili ya kupanua mawasiliano na kufafanua mfumo wa fikra wa Mapinduzi ya Kiislamu.”
Maoni yako